Irene Temu
Katavi
Wananchi wa Mkoa wa Katavi wamekuwa na dhana potofu juu ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu wakiamini ugonjwa huo unatokana na kulongwa hali ambayo imekuwa ikisababisha kushindwa kupatiwa matibabu kwa wakati kabla ya Ugonjwa haujakomaa
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Kudhibiti Ugonjwa Kifua Kikuu na Ukoma Manispaa ya Mpanda Bruno Cronely wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari wa vyombo mbambali wa Mkoa wa Katavi Juu ya Kuandikia,Kutangaza na kuripoti maswala ya ugonjwa wa TB yaliofanyika kwenye Ukumbi wa Kichangani katika Manispaa ya Mpanda .
Amebainisha kuwa baadhi ya wananchi kukosa uelewa juu ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB)imekuwa sababu ya wanaougua ugonjwa huo kuamini wamelogwa kitu ambacho sio sahihi katika afya ya binadamu .
Alisema kuwa Ugonjwa wa Kifua Kikuu hauenezwi kwa njia za kishirikina bali ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya hewa ambayo hupelekea mgonjwa wa ugonjwa huu kukohoa kikohozi kikali na kikavu kwa muda wa wiki mbili na kuendelea.
Cronel amesema kuwa mafunzo hayo waliopatiwa Waandishi wa Habari yatasaidia kuwa mabalozi wazuri kwa kuelimisha kwa ufasaha Jamii kuhusu Ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Amefafanua kuwa Manispaa ya Mpanda kwa mwaka 2019 walipanga kuwaibua wagonjwa 340 hata hivyo wameweza kuvuka lengo na kuwaibua wagonjwa 435 ambao ni sawa na asilimia 127.
Kati ya wagonjwa hao idadi ya waliofariki dunia ni wagonjwa 23 hali inayoonyesha kuwa ugonjwa huo sio wa kupuuzia hata kidogo kwani umekuwa ukisababisha vifo vya watu katika Jamii.
Kwa hapa nchini mwaka huo wa 2019 Jumla ya watu 137,000 waliugua ugonjwa wa TB ambao kati yao watu 81,000 walianzishiwa Matibabu ya Dawa sawa na asilimia 59 ambao kati ya watu hao watu 74,000 walitibiwa na kupona kabisa.
Amewataja waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Kifua Kikuu ni makundi ya wazeee, watoto na waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi na ameitaka jamii kuwa na utamaduni wa kufika kwenye vituo vya afya vya serikali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo pindi wanapokuwa wamehisi dalili za kuwa na Ugonjwa Kifua Kikuu.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa huduma za Jamii kutoka Amref Keneth Simbaya alisema wamechagua kundi la Waandishi wa Habari kuwapatia elimu hiyo ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB)kwa kuwa wana nafasi kubwa kupitia vyombo vyao vya habari kuifikia Jamii.
"...... naamini jamii ya watu wengi haifikiwi vya kutosha na kufahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu hivyo kwa kupitia mafunzo haya tuliyowapatia Waandishi wa Habari wataisaidia serikali katika mpango wake wa kukomesha Ugonjwa wa Kifua Kikuu hapa nchini ifikapo mwaka 2030.
Simbaya amesisitiza kuwa wao kama Amref wanatowa Maudhui kwa Waandishi wa Habari ili wafanye kazi kwenye jamii kwa kujikita katika utatuzi wa tatizo la ugonjwa huo kwa kushirikisha wataalamu wabobevu katika eneo hilo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mwandishi wa Habari Uhuru Media Irene Temu alisema kuwa jamii nyingi zimekumbwa na ugonjwa huo kwa kutojua chanzo na matibabu hivyo mafunzo aliyoyapata yataikomboa jamii kwa kuwapa Elimu kupitia chombo chake Cha Habari.
Zilipa Joseph Mwandishi wa ITV Mkoa wa Katavi kupitia mafunzo hayo amepongeza na kusema yamekuja kwa wakati sahihi kutokana na baadhi ya jamii kuwa na dhana potofu kuhusiana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na ameahidi Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Katavi watajikita kuelimisha jamii kupitia vyombo vyao mbalimbali vya habari .
