| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad |
Na Walter Mguluchuma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limemkamata Mamshi Abagashi Seleko(33) Raia wa Nchi ya Ethiopia akiwa ameingia nchini bila kibali kwa kutumia gari akielekea katika Mji wa Mpanda .
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ali Makame Hamad amewaambia Waandishi wa Habari kuwa raia huyo wa kigeni alikamatwa na Jeshi la polisi Mkoa wa Katavi wakati lilipokuwa likifanya msako kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika kijiji cha Mirumba Tarafa ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi akiwasafarini akitumia gari lenye namba za usajiri T.743 DMA aina ya Toyota Land cruiser V-8 VX mali ya Mwaipopo Mark Mkazi wa Dares salaam.
Kamanda Hamad alieleza baada ya tukio hilo dereva wa gari hilo alitoroka na kutokomea kusiko julikana na kumwacha raia huyo wa kigeni akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi .
Juhudi za kumsaka dereva huyo na Mmiliki wa gari hilo zinaendelea kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Katavi.
Mtuhumiwa huyo baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi amekabidhiwa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Katavi kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika tukio jingine Kamanda Ali Makame Hamad amesema watu wawili waliofahamika kwa jina la Faines Mihani(37) na Elizabet Nyandwi (13) mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Mlibanzi wamefariki dunia hapo hapo baada ya kupigwa na radi wakati wakiwa shambani wanalima.
Amesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Mlibanzi Kata ya Ipwaga Mishamo Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Tanganyika.