WATANO WAFARIKI KWA KUPIGWA NA RADI KATAVI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi akiwa kwenye eneo la nyumba ambayo watu watano wa familia moja wamefariki dunia baada ya kupigwa  na radi wakati wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao katika kijiji cha Kamsisi Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele(Picha na Walter Mguluchuma)

Na Irene Temu

Katavi

Watu watano wafamilia moja katika Kitongoji cha  Magulio Kata ya Kamsisi Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wamefariki baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha siku hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad ameeleza kuwa mnamo Mach 3,2022 majira ya saa Nne usiku watu watano wa familia moja walipigwa na radi nyumbani kwao wakiwa wamelala katika chumba kimoja na kufariki.

Nyumba ya nyasi waliokuwa wakiishi watu watano wa familia moja waliofariki dunia wakiwa wamelala kwa kupigwa na radi katika kijiji cha Kamsisi Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele nyumba hiyo ya nyasi imeungua baada ya radi kupiga na kuuwa watu hao watano wa familia moja(Picha na  Walter Mguluchuma)


Aidha Kamanda Hamad amesema waliofariki katika tukio hilo ni Masalu Sengule(32)Muri Shija(25),Nkiya Masalu(7),Vumi Masalu(5),Mariam Masalu(miezi mitano) wote wakazi wa Kijiji cha Kamsisi Tarafa ya Inyonga. 

Miili ya Marehemu hao tayari imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Sambamba na tukio hilo katika Kijiji cha Mlibanzi kata ya Ipwaga Wilaya ya Tanganyika watu wawili waliofahamika kwa jina la Faines Mihani(37) na Elizabeth Nyandwi(13) Mwanafunzi wa darasa la Sita katika Shule ya Msingi Mlibanzi walifariki kwa papo hapo baada ya kupigwa na radi wakiwa shambani wanalima.

Kamanda Hamad ameeleza tukio hilo limetoke Februari 28,2022 majira ya saa Tisa katika Kijiji cha Mlibanzi Kata ya Ipwaga Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Tanganyika na miili ya Marehemu baada ya uchunguzi imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa kupitia Kamanda wake ACP Ali Makame Hamad ametoa wito kwa Wananchi katika kipindi  hiki mvua zinapoendelea kunyesha kujiepusha kukaa katika maeneo hatarishi kama vile chini ya miti mikubwa ili kujiepusha na madhara ya mvua kwa kupigwa na radi.

Baada ya tukio la watu watano wa familia moja kupingwa na radi na kufariki papo hapo kwenye kijiji cha Kamsisi Kata ya Inyonga Wilayani Mlele  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ally Makame  Hamad akiwaeleza wananchi wa kijiji cha Kamsisi wasihusishe tukio la watu hao kufariki kwa kupigwa na radi kuwa imetokana na ushirikina(Picha na Walter MguIuchuma)



Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages