| Picha na Mtandao |
George Mwigulu na Paul Mathias,Mpanda.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wameiomba serikali ya Mkoa huo kuingilia kati mgogoro wa ardhi wa zaidi ya hekari 40 zilizopo katika Kitongoji cha Jelemanga “A” na “D” kijijini cha Milala.
Mgogoro huo uliodumu muda mrefu unatokana na baadhi ya wananchi kudai kuchukuliwa maeneo yao na serikali ya kijiji cha Milala na kugawiwa kwa wawekezaji mbalimbali kinyume na utaratibu wa sheria.
Miongoni mwa walalamikaji John Alex Wangala akizungumza jana akiwa kwenye eneo la mgogoro wa ardhi kijijini hapo alisema kuwa anashangaa kuona eneo lao likigawiwa kwa watu na kufanyika ujenzi wa nyumba za makazi pamoja huduma za kijamii kama vile kanisa,shule ya mtu binafsi huku wakiwa hawajui taratibu zipi zimetumika kupewa maeneo hayo.
Wangala alifafanua kuwa baada ya kufuatilia kwenye uongozi wa serikali ya kijiji cha Milala,Wenye mamlaka ya kijijini walishidwa kutoa ufafanuzi huku wakidai kuwa maeneo hayo niya wazi na kuwa ni mali ya kijiji.
Wakati hayo yakiendelea Wangala kwa kushirikiana na wananchi wengine wanaodai kuwa na uhalali wa umiliki wa maeneo hayo licha ya kuonesha nyaraka mbalimbali za kimaandishi zinazoonesha uhalali wa umiliki bado serikali ya kijijini imeshindwa kutambua uhalali huo.
Lwenche Erenest aliweka wazi kuwa baada ya kuona hakuna msaada wanaopewa na serikali ya kijiji waliamua kwenda Baraza la ardhi la Kata ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda pamoja na Mahakamani ambapo vyombo hivyo vya utoaji wa haki viliamuru eneo hilo kusitishwa uendelezaji wa shughuli zozote (Stop order) hadi pale ufumbuzi utakapo patikana.
“hatuwezi kukubali kupoteza haki yetu kwa njama zozote zinazofanywa na serikali ya kijiji na wawekezaji dhidi yetu,Tuna uhalali wa umiliki wa ardhi hii kwa sababu nyaraka tunazo tena ambazo zingine zimetiwa saini na viongozi wa serikali ya kijiji cha Milala Novemba28,2010 ambapo mihutasari inayoonyesha uhalali wetu wa umiliki…hatukubali viongozi watugeuke” alisema Erenest.
Anthony Mzoka alisema kwa kukiri kuwa alinunua moja ya sehemu ya ardhi ya mgogoro ambapo aliuziwa na serikali ya kijiji (kiasi cha fedha hakuweka wazi) lakini baada ya kuona linamgogoro aliweza kuondoka huku akishangaa kwanini serikali ya kijiji inaendelea kuuza maeneo hayo.
Mzoka aliiomba serikali ya kijiji hicho kuingilia kati mzozo huo wa ardhi kwani kama viongozi waliowapa dhamana ya kuwaongoza wanapaswa kutenda haki kwa wananchi wote huku akiiomba serikali ya Mkoa kutatua kero hiyo isije kuhatarisha usalama wa watu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Milala Veronica Lemi alikiri kuwepo kwa mgogoro wa ardhi ambapo kama serikali hatua ilizozichukuwa ni pamoja na kusitisha zoezi la upimaji ambao uliwahi kuendeshwa ili kuacha ufumbuzi upatikane.
Lemi akijibu madai ya serikali ya kijiji kuhodhii maeneo hayo bila utaratibu maalamu alisema kuwa historia inasema kuwa baadhi ya Babu zao wamiliki wa maeneo hayo waliondoka kijijini hapo mnamo mwaka 1960 ambapo mwaka 1970 kulifanyika operesheni ya upangaji wa vijiji na eneo hilo la ardhi liliangukia kuwa miliki ya serikali ya kijiji.
Aidha mwenyekiti huyo alisema serikali ya kijiji kwa sasa inautayari wa kusikiliza shauri la madai ya baadhi ya wananchi hao ingawa hakuna hati yoyote iliyowasilisha ofisini kwake ya zuio la uendelezaji wa shughuli za kibinadamu.
Diwani wa Kata ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda,Matondo Kanyepo alieleza kuwa anafahamu mgororo huo na wako katika hatua za kuutatua.
Kanyepo ameomba pande zote mbili kuvumilia wakati suluhisho la mgogoro huo ukiendelea kutafutiwa mwarobaini kila mmoja aweze kupata haki yake.