![]() |
| Madiwani wa Manispaa ya Mpanda wakiwa kwenye kikao Cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda. |
Katavi.
Diwani wa Kata ya Mwamkulu Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Kalipi Katani amefikisha kilio cha wananchi wa Kata yake mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Mpanda juu ya wananchi wake kukesha kwenye mashamba wakilinda mazao yao wakihofia kumalizwa na wanyama aina ya Kiboko ambao wamekuwa tishio kwenye Kata ya Mwamkulu
Diwani Kalipi alifikisha kilio hicho mbele ya Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Mpanda kilichofanyika jana kwenye Ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Mpanda uliopo Mtaa wa Ilembo na Kikao hicho kiliongozwa na Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry.
Alisema wananchi wamehama kwenye nyumba zao na kuacha kulala ndani ya nyumba na badala yake wamekuwa wakikesha kwenye mashamba hasa ya mbunga wakilinda mazao yao wakihofia kuliwa na kiboko ambao wamekuwa wakizagaa na kuwa tishio kwa wananchi .
Kalipi amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya ekari 20 za mazao yameliwa na kiboko ambao wamekuwa wakitembea usiku kwenye mbuga za mpunga za wakulima.
Alisema watu wamejenga nyumba kwa ajili ya kuishi na kulala sasa nyumba hizo zimekuwa zikilala wazi kutokana na wenye nyumba hizo kulala kwenye mashamba yao wakiyalinda dhidi mnyama kiboko.
Aliomba Idara husika ya Maliasili kufanya utaratibu wa kuwadhibiti viboko hao kabla ya kuleta madhara makubwa kwa wakazi wa Kata hiyo ambao wanaishi kwa kuhofia wanyama hao aina ya viboko .
Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry alisema kuwa tatizo hilo la viboko kuvamia kwenye makazi ya watu na kuharibu mazao lipo pia kwenye Kata yake ya Makanyagio hivyo ni vema maeneo yote yenye matatizo hayo yakatambulika.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Sofia Kumbuli alisema kuwa swala hilo la viboko watalifikisha Idara ya Maliasili ya Halmashauri ya Nsimbo ili kuwaomba wafanye operesheni ya kuwaondoa wanyama hao.
Manispaa ya Mpanda haina Idara ya Maliasili ndio maana wanalazimika kuomba msaada kwenye Halmashauri ya jirani ya Nsimbo .

