Na Walter MguIuchuma
CHAMA cha NCCR MAGEUZI Mkoa wa Katavi kimeunga mkono maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho juu ya kumsimamisha Uongozi Mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia na Makamu wake Anjelina Mtahiwa na kulaani vikali kundi linalomuunga mkono Mbatia na kupita Mikoani kuwashawishi viongozi wa Mikoa wa NCCR MAGEUZI kupinga uamzi wa Halmashauri Kuu.
Tamko hilo limetolewa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya NCCR MAGEUZI Mkoa wa Katavi kilichofanyika kwenye ofisi za Chama hicho na kuwashirikisha viongozi wa Majimbo Matano ya Mkoa wa Katavi.
Akitoa tamko la Chama hicho mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Kamishna wa Chama Cha cha NCCR MAGEUZI Mkoa wa Katavi Rajabu Makana alisema wanaunga mkono uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho iliyoketi tarehe 21 mwezi Mei mwaka huu na kutowa uamuzi wa kumsimamisha Uongozi Mwenyekiti wao wa Taifa James Mbatia na Makamu wake .
Alisema kuwa kwenye kikao hicho Mbatia alituhumiwa kutumia vibaya mali za chama na kudhalilisha viongozi wanawake ndani ya chama hicho na kushindwa kufanya kazi na viongozi wenzake .
Alibainisha kuwa Halmashauri kuu haina uwezo wa kusikiliza tuhuma za Mwenyekiti na kutowa maamuzi hivyo iliamua kuwasimamisha Uongozi Mwenyekiti na Makamu wake mpaka hapo mkutano mkuu wa chama hicho utakapo sikiliza utetezi wao juu ya tuhuma hizo .
Alisema kuwa chama hicho Mkoa wa Katavi kinazotaarifa za kuwa kuna watu wanaozunguka mikoani kwafuata wajumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa walioshiriki kupitisha uamuzi wa kuwasimamisha Uongozi James Mbatia na Makamu wake ili wasaini nyaraka za kukana kushiriki kwenye kikao kilichotoa uamuzi wa kuwasimamisha Viongozi hao.
Makana alisisitiza kuwa wao kama Viongozi wa Mkoa wa Katavi kwa niaba ya wanachama wao wanapinga kitendo hicho na kama Viongozi hao ni wasafi wasubiri Mkutano Mkuu badala ya kuendelea kuongeza makosa ya kudharau vikao halali vilivyotoa uamuzi wa kuwasimamisha Uongozi ndani ya chama hicho.
Nahivyo wao kama viongozi wa chama hicho wa Mkoa wa Katavi wataendelea kuunga mkono maamuzi yaliotolewa na Halmashauri kuu ya Taifa hadi hapo mkutano mkuu utakapotoa maamuzi tofauti na hayo.
Nae Mwenyekiti wa NCCR MAGEUZI Jimbo la Mpanda Mjini Abdul Sigera amesema kuwa amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa muda mrefu hivyo anaunga mkono uamuzi uliotolewa wa Halmashauri kuu yao ya Taifa.
Aliomba uitishwe mapema Mkutano Mkuu wa Taifa kwani ndio wenye uamuzi wa mwisho wa kumweka Mwenyekiti mwingine mpya ili chama kiendelee kufanya kazi na kupiga hatua kwa ajili ya kujiandaa na chaguzi zijazo za serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Nae Milton Mvilabo Mwenyekiti wa NCCR MAGEUZI Wilaya ya Tanganyika alipongeza Kikao kilichofanya uamuzi wa kuwasimamisha viongozi hao na kuongeza wao Viongozi wa Mkoa wa Katavi hawapo tayari kuwaunga mkono wanaozunguka kuwashawishi watu wamuunge mkono Mbatia na watakapofika Mkoa wa Katavi hawatakuwa tayari kuwasikiliza.

