Na Walter Mguluchuma.
Katavi .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewataka waendesha piki piki(BODA BODA) na waendesha Bajaji kutotumiwa kushiriki kwenye matukio ya kufanya vitendo vya uhalifu kwa kuwabeba wahalifu kwenye vyombo vyao vya usafiri au kuwakodishia watu wanaofanya uhalifu.
Mwanamvua ametowa maagizo hayo wakati alipokuwa akikabidhi Bajaji nane na piki piki tatu zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 81 zilizotolewa mkopo kwa waendesha boda boda na waendesha bajaji ikiwa ni mkopo uliotolewa na Benki ya NMB wenye kulenga kupunguza tatizo la vijana wasio na ajira ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Alisema kuna tabia ya baadhi ya boda boda na waendesha bajaji vyombo vyao kutumika kwenye matukio ya uhalifu kwa kuwabeba wahalifu au kuwakodishia usafiri wa vyombo vyao .
Hivyo aliwasisitiza watumie vyombo vyao vizuri kwa ajili ya lengo lililokusudiwa la kufanyia shughuli za kufanyia usafirishaji na wafanye shughuli hiyo kwenye maeneo yote ya Mji wa Mpanda bila kuwakodishia watu kufanyia uhalifu .
Alisema NMB wamefanya kazi kubwa ya kutowa mikopo hiyo na inaonyesha jinsi ambayo inaiunga mkono Serikali kwenye kupunguza tatizo la watu wasio na ajira hapa nchini kwani Serikali imekuwa ikisisitiza kila mtu kufanya kazi .
".....hakikisheni vyombo hivyo mlivyokopeshwa mnavitumia kwa kuzingatia sheria za usalama bara barani vinginevyo kama hamtotii na kuzingatia sheria za usalama barabarani mtakuwa mnatishia amani"alisema Mrindoko
Amewata pia waendesha boda boda kufanya kazi kwa bidii ili mkopo huu waliokopeshwa na NMB waweze kuurudisha kwa wakati na hata hapo baadaye kununua vyombo vikubwa zaidi ya hivyo kwani Mkoa wa Katavi bado una mahitaji ya vyombo vya usafiri
![]() |
| Baadhi ya wadau waliohudhuria hafla ya kuwakabidhi Dereva Boda Boda na Bajaji mkopo wa Pikipiki na Bajaji uliotolewa na Benki ya NMB tawi la Mpanda Mkoa wa Katavi.(Picha na Walter MguIuchuma) |
Meneja mauzo wa NMB Kanda ya Magharibi Trifon Melkiory alisema benki hiyo inaendelea kushirikiana na waendesha boda boda kwa kuwapatia mikopo kwa kupitia mpango wa MASTABODA .
Alisema kuwa hadi sasa Mkoa wa Katavi umekuwa na mwitikio mkubwa katika mpango huu na unaongoza kwa kupatiwa mkopo huu ukifatiwa na Mkoa wa Tabora ambao hadi sasa wamekopeshwa bajaji sita wakati Mkoa wa Katavi wamekopeshwa bajaji nane na pikipiki tatu .
Mlezi wa Boda boda na Waendesha Bajaji wa Mkoa wa Katavi Beda Katani alieleza kuwa mkopo huo waliopatiwa wasidhani kuwa ni wabure wahakikishe wanarejesha NMB mkopo huu kwa mujibu wa mkataba wao na benki hiyo ili na wengine waweze kunufaika na mkopo .

