
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko
Na Mwandishi wetu,
Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi kuhakikisha ndani ya Siku 35 kuanzaia Juni 27,2022 anawachukulia hatua watumishi wote waliokula kiasi cha Tsh. Milioni 33.4 pesa za ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa POS.
RC Mrindoko ametoa agizo hilo katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda lililofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa wakati wa kupitia na kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) katika kikao hicho.
Alisema wale wote waliohusika na upotevu wa Fedha hizo wafanyiwe mahojiano sambamba na fedha hizo kurejeshwe ifikapo August 2,2022 na kupatiwa taarifa ya fedha zote kurejeshwa kwenye Halmashauri.
"ikifika tarehe hiyo kama fedha hizo hazijarudishwa basi wahusika wote wafunguliwe mashtaka ya uhujumu uchumi kwani hawawezi kujinufaisha kwa fedha za mapato kutoka kwa Wananchi wanaopambana usiku na mchana"alisisitiza Mrindoko
Aidha ameagiza hoja zote takribani asilimia 63% ambazo hazijafungwa zipatiwe majibu ndani ya mwezi mmoja na kuwasilishwa kwa Mkaguzi wa nje ili hoja hizo ziweze kufungwa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Mwanamvua Mrindoko ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa kupata hati safi (Unqualified Opinion) kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.