JELA MIAKA 20 KWA KUPATIKANA NA MENO YA TEMBO YENYE ZAIDI YA MILIONI 52.




Picha kwa msaada wa BBC News/Swahili

Na Walter Mguluchuma ,Katavi

Watu wawili wakazi wa Kijiji cha Itenka Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi Beno Msimbe na Nova Mazeba wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na meno mawili ya Tembo yenye Thamani ya Tshs Milioni 52.948,540.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi Gway Sumaye baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Gway Sumaye aliiambia Mahakama kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo,upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na meno hayo ya Tembo siku hiyo ya tukio.

Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka,watuhumiwa wote wawili wamepatikana  na hatia kinyume cha sheria kifungu 86(1) na 2(b) cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Na 5 ya Mwaka 2009 na kifungo cha 60(2) cha sheria ya uhujumu Uchumi sura ya 200 ya Mwaka 2019.

Hivyo alitoa nafasi kwa washitakiwa endapo wanasababu yoyote ya Msingi itakayoweza kuishawishi Mahakama iweze kuwapunguzia adhabu.

Washitakiwa katika utetezi wao waliiomba Mahakama iweze kuwapunguzia adhabu kwa kuwa wanafamilia zinazowategemea wao.

Hata hivyo maombi hayo yalipigwa vikali na mwendesha mashitaka ambaye ni Mwanasheria wa Serikali Lugano Mwasubila ambaye aliiomba Mahakama itowe adhabu kali kwa washitakiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuhujumu uchumi wa nchi.

Hakimu Mkazi Gway Sumaye baada ya kusikiliza maombi ya washitakiwa na upande wa mwendesha mashitaka alisoma hukumu na kuiambia Mahakama kuwa kutokana na kosa walilopatikana  nalo washitakiwa Beno Msimbe na Nova Mazeba Mahakama imewahukumu washitakiwa wote wawili kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Awali Kwenye kesi hiyo mwendesha mashitaka Mwanasheria wa Serikali Lugano Mwasubila alidai kuwa washitakiwa hao walidaiwa kutenda kosa hilo mnamo Februari 10 Mwaka huu huko katika Kijiji cha Itenka Wilaya ya Mpanda.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages