BILIONI 148 UJENZI UMEME WA GRIDI YA TAIFA KUTOKA MKOA WA TABORA-KATAVI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Phillip Mpango akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Katavi katika ziara yake Mkoani humo.

Na Mwandishi wetu,Katavi

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt.Phillip Isdor Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha hadi kufikia Oktoba 2023 Mkoa wa Katavi unapata umeme wa uhakika.

Ameyasema hayo akiwa ziarani mkoani Katavi katika viwanja vya Shule ya Msingi Inyonga iliyopo Halmashauri ya Mlele mara baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha Inyonga.

Dkt. Mpango amesema Hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa umeme wa Gridi ya Taifa ulioanza mwaka 2019 ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 12.

"Naibu Waziri mpelekee salamu Waziri,hebu angalieni upya utaratibu wenu wa kubadilisha nguzo za miti nakwenda kuwa nguzo za zege, umejinyonga mwenyewe Oktoba 2023 sitaki kiswahili wala kisingizio,Mkoa wa Katavi uwe umeunganishwa na gridi ya Taifa" Alisema nakuongeza

"Mmeshachelewa miezi nanane kujenga hiki Kituo mfanye juu chini mfidie hiyo miezi minane, ninachotaka wananchi wapate umeme wa uhakika, Wizara ya Nishati na Tanesco hakikisheni ujenzi unakamilika, ningekuwa mimi ningejiwekea lengo la kabla ya hapo".

Hata hivyo ameitaka Wizara hiyo kuharakisha uthamini wa mali za wananchi watakao athirika na ujenzi wa njia hiyo kulipwa fidia kwa wakati.

"Mheshimiwa Naibu Waziri uwatake Tanesco kabla ya huu mradi wawe wanakupatia maendeleo ya huu mradi kila baada ya miezi mitatu kwa sababu sitaki tena kisingizio" alisema

Aidha,kwa kuwa Mkoa wa Katavi unategemea umeme unaozalishwa kwa mafuta na mashine za jenereta na kupelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara Dkt.Mpango ameitaka Wizara ya Nishati kuleta Jenereta lililopo Loliondo kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alisema umeme unaozalishwa katika Mkoa wa Katavi ni megawati 6 wakati mahitaji ni megawati zaidi ya 7 hivyo kupelekea Mkoa kukosa wawekezaji kutokana na upatikanaji mchache wa umeme.

Awali Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato alisema sababu za kuchelewa kwa mradi huo ni tatizo la UVICO-19,mzabuni wa ununuzi kushindwa kununua vifaa kutokana na bei ya soko kuwa juu na pia mzabuni wa ujenzi Electrical Transmission and Distribution Company (ETDCO) kuchelewa kuanza ujenzi bila sababu ya msingi.

Hata hivyo pamoja na sababu hizo Naibu Waziri Byabato alimuahidi makamu wa Rais kuwa hadi kufikia Oktoba 2023 mradi huo utakuwa umekamilika.

Akitoa taarifa Meneja wa Mradi Eng. Sospeter Oraro alisema mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msingi wa kilovoti 132 kutoka Tabora-Katavi (383km) pamoja na vituo ya kupooza umeme vya Ipole, Inyonga na Mpanda  umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 148 na uko nyuma kwa miezi 8 kutokana na sababu mbalimbali.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages