MIUNDO MBINU YA BARABARA TANROADS KATAVI YAHUJUMIWA.

 

Wanafunzi wa Shule ya sekondari Misunkumilo Manispaa ya Mpanda wakionyesha nguzo ya taa iliyoibiwa na kutelekezwa shuleni hapo kitendo kilichofanya na Wananchi wasio wazalendo.(Picha na Walter MguIuchuma)

  Na  Walter  Mguluchuma,Katavi.

WAKALA  wa Barabara  Tanzania  (TANROADS) Mkoa wa Katavi  imewaonya watu wanaofanya hujuma za kuharibu miundo mbinu ya barabara kwa kuiba taa za barabarani  kwani kufanya hivyo ni kuhujumu Serikali ambayo imetumia fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza miundo mbinu hiyo ya Barabara.


Onyo hilo limetolewa na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Katavi Mhandishi Martin Mwakabende kufuatia watu wasiofahamika kuhujumu miundo mbinu ya barabara kwa kuiba taa tatu za barabarani zenye thamani ya zaidi ya   shilingi milioni kumi huko katika eneo la Misunkumilo Manispaa ya Mpanda kwenye barabara ya kutoka Mpanda  Mjini kueleke Vikonge hadi  Kigoma. 

 

"Serikali imetumia zaidi ya  Tsh Bilioni 1.8 kuweka taa za barabarani kwenye barabara hiyo ya kuanzia Mpanda Mjini,vikonge hadi Kigoma  lakini inashangaza watu wameanza kuharibu miundo mbinu kwa kuiba taa za barabarani nawaambia watambue kuwa kufanya hivyo wanahujumu  jitihada za Serikali za kuboresha miundo mbinu kwa wananchi"alisema Mhandisi Mwakabende

 

Amebainisha pia wizi huo uliotokea usiku wa kuamkia Julai  27 majira ya saa nane na nusu tayari wameshalijulisha Jeshi la Polisi juu ya kufanyika kwa hujuma  hiyo hivyo wanaendelea na uchunguzi wa kuwabaini watu waliohusika na tukio hilo.

 

Mwakabende amewaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuweza kuwabaini watu wote wanao husika kuhujumu miundo mbinu ya barabara kwani zinamanufaa kwa wananchi wote  wanao tumia barabara na wale wasio tumia barabara.

 

 Mwenyekiti wa Mtaa wa Misunkumilo  Katavi Joseph amesema kuwa yeye alipata taarifa za tukio hilo majira ya saa nane na nusu usiku wa kuamkia julai 27 kuwa kuna taa za barabarani zimeibiwa  kwenye eneo la Mtaa wake .

 

Alisema taarifa hizo alizipata kupitia kwa walinzi shirikishi  waliokuwa wakilinda kwenye Mtaa huo usiku na kuungana nao kufuatilia wahalifu waliotekeleza tukio hilo na kufanikiwa kuikuta taa moja ikiwa imekatwa nguzo na kuegeshwa kwenye eneo la Shule ya Sekondari Misunkumilo ikiwa na sola yake huku wahalifu wakikimbia baada ya kugundua wanafuatiliwa.

 

Mwenyekiti huyo  alisema ilipofika asubuhi iliwalazimu kuomba msaada wa   wanafunzi wa Sekondari ya Misunkumilo ili wawasaidie kuendelea kutafuta sola na nguzo nyingine kwenye pori  lililokaribu na shule hiyo na ndipo waliweza kufanikiwa kukuta  nguzo nyingine ya  sola ya umeme ikiwa tayari imekatwa katwa vipande  na sola yake pembeni yake.


Baadhi ya vipande vya nguzo za taa za barabarani zilizoibiwa na watu wasiojulikana na kutelekezwa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi.


Afisa Mtendaji wa Kata ya Misunkumilo  Mussa Athuman alisema kuwa taarifa za tukio hilo alipata kutoka kwa Mwenyekiti wake wa Mtaa wa Misunkumilo ambapo nae alitowa taarifa kwa   Tanroads ambao waliweza kufika kwenye eneo hilo kwa wakati.

 

 Alieleza  kuwa taa hizo zimekuwa na msaada mkubwa kwa wananchi kwani hapo awali  kwenye eneo hilo kulikuwa na matukio ya   watu kuporwa mali zao lakini toka taa zimewekwa matukio hayo yametoweka hivyo  uongozi wa Kata hiyo  utaendelea kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na wananchi pamoja na Jeshi la Polisi kuwabaini wanao taka kuharibi miundo mbinu hiyo ya Barabara.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages