Wafanyabiashara wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zao kwa ufanisi yaliyotolewa na Benki ya NMB Mkoa wa Katavi |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Benki ya NMB imewapatia mafunzo Wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zitakazo wanufaisha na kuwapatia wateja wa aina mbalimbali na kuinua kipato chao na uchumi wa Mkoa huo kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wafanya biashara hao yamefanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda ulipo eneo la Kota za Madini na yaliwashirikisha Wafanyabiashara wote kutoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Katavi.
Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Benki ya NMB Sospeter Magesse alisema kuwa NMB wapo Katika Mkoa wa Katavi kwa lengo la kuhakikisha Wafanyabiashara wa aina zote wanakuza biashara zao na ndio maana wameamua kuwapatia mafunzo yatakayo wanufaisha kwenye biashara zao mbalimbali wanazofanya .
Amebainisha kuwa wamekuwa wakitowa mikopo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia Wafanyabiashara na ndio maana wameanzisha pia mikopo ya wakulima na wafugaji , wavuvi,wachimbaji na wakandarasi lengo ikiwa ni katika kumwinua Mfanyabiashara wa hali ya chini,wakati na wa hali ya juu.
Magesse aliongeza kuwa wao NMB wanaimani kuwa mafunzo hayo waliowapatia Wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi yatawasaidia kuboresha biashara zao na kuzikuza pia.
Upande wa sekta ya kilimo Benki hiyo ya NMB alieleza kuwa inakitengo kinachoshughulikia na wanatowa mikopo kwa ajili ya zana za kilimo na ili mkulima aweze kukopeshwa zana za kilimo anatakiwa kuchangia asilimia 20 ya bei ya zana hizo.
Amefafanua kuwa mikopo hiyo pia hutolewa kwa kiwango hicho hicho kwa wateja wenye sifa za kukopesheka na wanaweza kukopa magari zana za kuchimbia madini , mitambo ya ukandarasi ,bajaji,vifaa vya uvuvi na vinginevyo .
Magesse amewataka Wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi kuwa na utaratibu wa kuweka bima za biashara zao kwani Wafanyabiashara wengi wa Mkoa wa Katavi biashara zao hazina bima .
Mwenyekiti wa Business Club wa Mkoa wa Katavi Raymond Kamtoni alieleza kuwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi wamekuwa wakinufaika na Benki ya NMB kwa mikopo ambayo wamekuwa wakiwapatia ambapo kwa sasa riba imepunguzwa tofauti na Benki nyingine .
Alisema kuwa miongoni mwa Wafanyabiashara walionufaika na mkopo wa mitambo ya kuchimbia dhahabu yeye ni mmoja wapo kwani mtambo aliokopeshwa unamsaidia kwenye shughuli zake na pia ameweza kuongeza ajira kwa vijana wanaofanya kazi kwenye mgodi wake .
Nae Mwezeshaji wa mafunzo hayo James Mwang'amba aliwasisitiza Wafanyabiashara kuweka fedha zao benki badala ya kuzihifadhi kwenye mitungi ndani ya nyumba zao kwani wanapo weka fedha Benki inakuwa ni rahisi kuweza kukopesheka na Benki yoyote.