Na Walteruluchuma
Mahakimu wa Mahakama za Mkoa wa Katavi wamepatiwa mafunzo ya uelewa wa pamoja kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali zilizofanyiwa marekebisho ya sheria ya mwaka 2020 ili wawe na uelewa wa pamoja kwa kuwa wao ndio watumiaji wa sheria hizo.
Naibu Msajili wa Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga Maira Kasonde alisema kwa sasa Mahakama ipo kwenye kipindi cha maboresho na moja ya mambo wanayoyafanya ni pamoja na kutoa elimu kwa watumishi wake wa kada mbalimbali kuanzia Majaji na Mahakimu.
Alieleza baada ya sheria mbalimbali kufanyiwa marekebisho mwaka huu Uongozi wa Mahakama umeona ni vema Mahakimu wote wakapatiwa elimu ya ulewa wa pamoja hivyo Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga imefanya Uzinduzi wa mafunzo hayo katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi na baada ya hapo watakwenda Wilaya ya Nkasi , Kalambo na hatimaye Sumbawanga Mkoa wa Rukwa.
Lengo Kuu la mafunzo hayo likiwa ni kuhakikisha Mahakimu ambao ni watumiaji wa sheria hizo wanakuwa na uelewa wa kutosha na wapamoja kuhusiana na mabadiliko yaliyojitokeza huku sheria zilizofanyiwa marekebisho zikiwa ni nyingi na ambazo wameziona muhimu wazipitie na kuzifanyia mafunzo ni sheria tatu.
Sheria hizo tatu zilizofanyiwa marekebisho na wanazo zifanyia mafunzo Kasonde amezitaja kuwa ni sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019, sheria nyingine ni ya kanuni ya adhabu sura ya 16 na sheria ya uhujumu uchumi ambayo nayo imefanyiwa marekebisho kupitia sheria namba moja ya Mwaka 2020.
"...…tumeamua kuwaita Mahakimu wote kwenye mafunzo hayo wakiwemo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kwa sababu kuna sheria zinazotumika mahakama za juu pekee lakini siku hizo mahakimu wanao ajiliwa lazima waanzie Mahakama ya Mwanzo ambapo hapo baadae huwa wanapanda hivyo ndio sababu tumeona washiriki Mahakimu wote ili kesho na kesho kutwa wajuwe ni nini kinacho hitajika"alisema Naibu Msajili Kasonde.
Alifafanua kuwa sheria hizo zinatumika pia kwenye mahakama zote kama vile sheria ya kanuni ya adhabu inatumika pia katika Mahakama ya mwanzo na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kuna baadhi ya vipengele vinatumika katika Mahakama za mwanzo na ambavyo vimeguswa kikiwemo kifungu cha 91 cha sheria hiyo kinacho mpa mamlaka DPP Kuondoa shitaka Mahakamani ndio maana wakaona watowe mafunzo kwa wote ili wawe na uwelewa wa pamoja.
Katika hatua nyingine kwenye mafunzo hayo mbali ya kuelimishana wamejadili pia changamoto zinazoibuka kuhusiana na sheria hizo na kuzipatia ufumbuzi na mafunzo hayo yamefanyika kutokana na maelekezo ya uongozi wa juu wa Mahakama.
Nae Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Katavi Fred Shayo amesema kuwa wamepitishwa kwenye mabadiliko mbalimbali ya sheria zilizorekebishwa mwezi Machi mwaka huu na kuzingatia sheria nyingi zinawahusu Mahakama .
Hakimu Shayo alitolea mfano sheria ya mabadilioko ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 toleo la mwaka 2022 imefanyiwa mabadiliko katika vifungu mbalimbali ikiwemo kifungu namba 131 kinaelekeza kwamba mashauri yote yanayofunguliwa Mahakamani lazima upelelezi uwe umekamilika kama upelelezi utakuwa hauja kamilika mahakama inauwezo wa kufuta kesi hiyo ili kuepukana na mrundikano wa mashauri mahakamani .
Nae Hakimu David Mbembele alisema kuwa marekebisho hayo ya sheria yamezipa uwezo Mahakama za chini kuwa na uwezo wa kutoa mdhamana kwa kesi za uhujumu uchumi mpaka dhamani ya chini ya shilingi milioni 300 ambapo hapo awali mahakama kuu ndio iliyokuwa na mamlaka hayo.