RAIS SAMIA AOMBWA KUNUSURU SEKTA YA TUMBAKU.

Mkulima wa zao la Tumbaku akiwa kwenye wakati wa mavuno wa zao hilo (Picha na Mtandao)

Ni baada ya kuibuka kwa vurugu, uvunjwaji sheria Kampuni za kigeni zajipanga kuiburuza serikali mahakama za kimataifa.

Na Walter Mguluchuma,Katavi.

Katika hali isiyo ya kawaida sekta ya tumbaku imekumbwa na vurugu zinazohatarisha amani na ustawi wa biashara ya zao hilo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa maofisa wa kampuni za ununuzi wa tumbaku (jina tunalo), amesema hali hiyo imesababishwa na matumizi mabaya ya madaraka na kuyumba kwa wasimamizi wa sheria inayoongoza kilimo na biashara ya tumbaku.

Kwa mujibu wa sheria, kampuni zote za tumbaku zilipaswa kuwasilisha makisio yao Bodi ya Tumbaku kabla ya Machi 1, 2022.

“Ni maelekezo ya bodi yaliyotolewa kwa barua ya Februari 7 mwaka huu. Kampuni nyingi ziliwasilisha makisio yao ya uzalishaji,” anasema.

Nakala ya barua hiyo yenye kumbukumbu Na. TTB/PM/1/VOL XIV/18 tunayo.

Anasema barua nyingine ya Bodi ni ya Juni 9 mwaka huu iliyoelekeza majadiliano ya kufunga mikataba baina ya wakulima kupitia vyama vya msingi na kampuni za ununuzi, ikiweka ukomo wa Juni 30, 2022.

Gazeti hili linafahamu kuwa kampuni zilizokuwa zikishiriki ununuzi wa tumbaku zilifanya hivyo na kusaini mikataba na vyama vya msingi kwa mujibu wa Sheria ya Tumbaku Na 34 ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2011.

“Kinachofanyika sasa ni serikali kuruhusu fujo zinazofanywa na kampuni inayojiita Mkwawa Leaf na AMY Holding kupita vyama na kutoa hongo kwa viongozi waandamizi na baadhi ya wakulima kushawishi vurugu,” amesema.

Anasema wafanya fujo hawa wanajinadi kuwa wametumwa na Waziri wa Kilimo na kwamba hawazuiliki licha ya kuwa Septemba 1, 2022, Bodi ilitoa barua kusisitiza kuwa ukomo wa kufunga mikataba ulikuwa Agosti 30, 2022.

“Hawajali na sasa wanavunja mikataba halali ya vyama na kampuni za ununuzi wa tumbaku. Kampuni ya Mkwawa imedirika hata kununua tumbaku za kampuni nyingine bila kuheshimu mikataba iliyopo kwa mujibu wa sheria,” anasema.

Ofisa huyo anasema wamekuwa wakiwashinikiza wateuzi wa tumbaku wa Bodi kwa kutumia Ofisi ya Waziri wa Kilimo, huku wakiitumia wizara kuchafua kampuni za kigeni zilizopo nchini ambazo zimesaidia sana kulinda soko la tumbaku nje ya nchi.

Anasema hali hiyo inaitia doa serikali kwa kudaiwa kunyanyasa kampuni za kigeni huku ikifanya uvunjifu mkubwa wa sheria zinazosimamia tumbaku na sasa kampuni za kigeni zinafikiria kufungua shauri katika mahakama za kitaifa.

“Pamoja na kuwa hatua hii ni mbaya sana kwa wawekezaji na serikali, lakini hatuwezi kukubali hasara inayojitokeza inayosababishwa na Kampuni moja tu yenye nguvu ya kuamrisha viongozi wa serikali na kuvunja sheria kwa kuwa ipo karibu na Waziri wa kilimo kama inavyojinasibu,” anasema huku akitoa mfano wa matukio yaliyotokea Kahama, Kaliua, Mpanda na yanayoendelea huko Chunya, akiyaeleza kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi walioaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amemsihi Rais na Waziri Mkuu kuingilia kati suala hilo kwani kwa hali ilivyo hakuna tena usimamizi wala usawa kwenye biashara hiyo na matokeao yake yatakuwa ni majuto kwa sekta kwa kipindi kirefu.

Ofisa huyo amehoji kama mifumo ya nchi imejiridhisha na uuzwaji wa mal zote za kampuni iliyokuwa TLTC, malipo ya kodi, mgawo wa hisa za wakulima kwenye kiwanda na majina halali ya Kampuni iliyonunua hisa hizo.

Amesisitiza kuwa hawataruhusu chama chochote kilichovunja mkataba kinyume na utaratibu kuuza tumbaku popote hadi watakapolipa fidia ya mkataba kupunguza hasara za kampuni hizo.

Ameomba Bodi ya Tumbaku ijitathmini kama inastahili kuendelea kusimamia zao au wamuachie Waziri afanye kila kitu kwa kulinda maslahi yake na wakaribu yake kama apendavyo.

 

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages