Na
George Mwigulu,Nsimbo.
Wachimbaji wa madini wa Kata ya Ibindi halmashauri ya wilaya ya Nsimbo Mkoa wa Katavi wameahidiwa na mbunge wa Jimbo la Nsimbo,Anna Lupembe kuwa atamwalika waziri wa Madini Dkt Doto Biteko kwenye halmashauri hiyo ili kuweza kuzungumza na wachimbaji hao kwa ajili ya kutatua kero zao na kupewa elimu ya fursa za uwekezaji.
Amesema hayo leo Mbunge huyo wakati akiwahutubia wananchi wa kata ya Ibindi kwenye ziara yake ya kikazi jimboni humo ambapo amefafanua kuwa anatambua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wachimbaji wa madini hasa wadogo wadogo.
Lupembe ameeleza kuwa serikali
ya awamu ya sita inadhamira njema kwa wananchi wake ya kuhakikisha wanapata
maendeleo ya kiuchumi kwa sababu hiyo imekuwa ikitengeneza mazingira rafiki ya
miundombinu bora ili kurahisisha upatikanaji wa fursa za kiuchumi.
Mbunge huyo amesema kuwa Waziri
wa Madini, Dkt Doto Biteko atafika ndani ya halmashauri ya Nsimbo na kuonana
moja kwa moja wa wachimbaji wa madini kwani licha ya kutatua kero zao bali ziko
fursa nyingi za kiuwekezaji kwenye sekta za madini ambazo wachimbaji wanapaswa
kuzifahamu.
Aidha anafahamu kuwa katika Kata ya Ibindi wako wawekezaji mbalimbali wa madini ambao wamekuwa wakifanya shughuri zao za kiuchimbaji hivyo ataendelea kuzungumza naoi li waweze kuendelea kushiriki kwenye kazi za maendeleo ya kata hiyo kama vile kuchangia fedha kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali.
Wananchi wa Kata ya Ibindi waliohudhuria kwenye mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Nsimbo,Anna Lupembe leo ambapo ameweza kuzungumza na wachimbaji wa madini pia. |
Nao baadhi ya wananchi wa kata
ya Ibindi wamemshukuru mbunge huyo kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwasaidia
wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya kuwakutanisha na waziri wa madini.
Amesema hayo Masaja Daudi
ambaye ni mchimbaji wa madini katika kata ya Ibindi ambapo ameeleza kuwa kama
wachimbaji wa madini wazawa watapewa fursa zaidi ya elimu ya uchimbaji wataweza
kupata tija kubwa kwenye uchimbaji.
Maulid Rashidi,Mchimbaji wa
madini amesema kuwa wanataka kuona rasirimali za taifa kama madini
yanawanufaisha zaidi wazawa na sio wageni pekee kwani itakuwa aibu kubwa
kuachiwa mashimo pekee na umasikini huku madini yakiwanufaisha watu wanje.