Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023,Abdallah Shaib Kaim akishuhudia hivi karibuni upimaji wa upana wa barabara ya Isinde Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi. |
Na George Mwigulu,Nsimbo.
MWENGE wa Uhuru mwaka 2023 umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa barabara ya kiwango cha lami mita 745 wenye thamani ya zaidi ya fedha Mil 491 katika kijiji cha Isinde kata ya Mtapenda halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi utakao hudumia jamii.
Barabara
hiyo ni sehemu ya mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa Km 511.18 za
halmashauri ya Nsimbo ambapo kati ya
hizo ni Km 2.14 ni lami,Km 111.308 ni changarawe na Km 397.622 ni za udongo.
Akiweka jiwe la msingi leo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2023.Abdalla Shaib Kaim katika kijiji cha Isinde Kata ya Mtapenda amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa miundombinu ya barabara nchini imekuwa ikitoa fedha nyingi za kujenga barabara zitakazo chochea ukuaji wa maendeleo ya wananchi.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuwa na nyaraka zote za ujenzi wa mradi wa barabara na miradi mingine yote kutokuwa na dosari yoyote.
Licha ya kuwapongeza na kuweka jiwe la msingi ametoa siku tano kwa uongozi wa halmashauri hiyo kufanya marekebisho ya barabara hiyo ya Mita 745 baada ya mwenge wa uhuru kubaini kuna mapungufu.
”Katika sehemu ambazo mwenge wa uhuru umebaini kuna chanamoto tunaagiza ndani ya siku 5,Na kwa kutambua mkandarasi bado yupo site aitwe aelekezwe na sehemu hiyo ifanyiwe marekebisho na baada ya kufanya marekebisho tunahitaji taarifa ya utekelezaj wa marekebisho pamoja na picha za kabla na baada na video wakati mkandarasi akiwa site ili kuona agizo lililotolewa na mwenge wa uhuru limetekelezwa kwa wakati ” Amesisitiza Kaim.
Vilevile amemwomba Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Jamila Yusuph kwa kushirikiana kamati ya ulizi na usalama ya wilaya kuona kwamba kwa sehemu hiyo na maelekezo hayo wanawasimamia TARURA sambamba na kuhakikisha ujenzi wote na muda wa matazamio ya mradi kuwa ubora na viwango wa ujenzi wa barabara umezingatiwa.
“Msisite popote kuchukua hatua mtakapo ona kuna changamoto wakati wa kipindi cha matazamio mhakikishe mnatoa maelekezo kwa ajili ya kurekebishwa mpaka muda wa matazamio utakapokamilika kwani rais Samia Suluhu Hassain anatmia fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kufaidika” Amesema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Awali Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpanda,Mhadisi Hoza Joseph akisoma taarifa ya mradi wa barabara hiyo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Abdalla Shaib Kaim amesema kuwa mradi wa barabara ya Isinde uliibuliwa na Wakala wa barabara Vijijini na Mjini (TARURA) mwaka wa fedha 2022/23,ukiwa na lengo la uboreshaji na uimarishaji wa barabara katika mji wa Nsimbo.
Mhadisi Joseph amesema ujenzi wa barabara ya lami ulianza kutelekezwa Septemba,2022 na kukamilika Feb,2023 kwa hatua ya ujenzi wa lami nyepesi na mifereji yam awe na kazi zilizobaki ni uwekaji wa alama za barabarani na usimikaji wa taa ambapo gharama ya ujenzi wa lami ni zaidi ya fedha Mil 491.
Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Anna Lupembe akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isinde Kata ya Mtapenda kabla ya kuweka kwa jiwe la msingi wa barabara hiyo. |
Mbunge
wa Jimbo la Nsimbo Mkoa wa Katavi,Anna Lupembe amesema kuwa serikali inafanya
kazi kubwa ya kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inajengwa katika Jimbo
la Nsimbo kama sehemu ya kuwahudumia
wananchi.
Lupembe
ameipongeza serikali kwa kuimarisha miundombinu ya barabara ambapo kwa sasa
mtandao wa barabara za lami unaendelea kuimarika.
Aidha
katika halmashauri ya Nsimbo umekimbizwa
Km 198 na kupitia jumla ya miradi 10 yenye thamani ya Fedha zaidi ya Mil 897.