George Mwigulu,Nsimbo.
Ukosefu wa maji safi salama kwa baadhi ya vituo
vya afya na zahanati katika halmashauri ya wilaya ya Nsimbo Mkoa wa Katavi ni
chanzo cha wanawake wajawazito wanaokwenda kujifungua kupewa jukuma la kuchota
maji.
Baadhi ya wanawake wakitoa kero zao hivi
karibuni kwa mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mkoa wa Katavi,Anna Lupembe wameeleza
kuwa wanapopata uchungu na kwenda katika zahanati za serikali baada ya kujifungua na kabla
hawajaruhusiwa kurudi nyumbani wanatakiwa kuchota ndoo tano za maji ikiwa kwa wakati
huo hawajapata nguvu.
Mariam Sayi,Mkazi wa kijiji cha Uruwila amesema kuwa kitendo cha
ukosefu wa miundombinu ya maji kwa baadhi ya zahanati za serikali kumekuwa kero
kwao na kuwa adhabu.
“Sasa
suala la kuzaa linaonekana kama adhabu kwetu,tunapitia mateso ambayo ni vigumu
kwa kiongozi wa ngazi ya wilaya kufahamu hilo kwa kuwa wao wanaishi kwenye mazingira
mazuri yenye maji ya kutosha” Amesema Mariam.
Hawa Lazaro anasema kuwa usubufu wanaoupata wa kuchota maji
unawafanya baadhi ya wanawake kutokwenda kwenye vituo vya afya na zahati za
serikali hivyo wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Manispaa ya Mpanda
kujifungua na kusabisha gharama kubwa ya kifedha ambapo hawawezi kumudu.
Ameiomba serikali ya halmashauri ya wilaya ya Nsimbo kuwaonea
huruma kwani wanaoteseka zaidi ni wanawake wanao kwenda kwenye vituo vya afya
na zahanati kujifungua.
Mtendaji wa Kata ya Uruwila,Revocatus Mapula amekiri kuwepo kwa
kitendo cha wanawake kupewa majukumu ya kuchota maji lakini kwa sasa hakipo
kutokana na kupiga marufuku Wauguzi wa afya kufanya hivyo.
“Nilimwita inchaji wa zahanati hiyo nikamwambia ni
marafuku mama yeyote akijifungua wewe umwagize akachote maji…huko nyuma kweli
lilikuwepo na kwa bahati nzuri kwenye kikao cha Isagala juzi tuliliongelea na
kulitolea ufafanuzi na Mh Diwani akakemea hilo,sasa kama linaendelea tunaomba
mtuletee ili tulishughulike” Amesema Mapula.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nsimbo,Mohamed Ntandu anasema serikali inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha maji yanafika kwenye maeneo ya zahanati kwa kutumia mtandao wa RUWASA.
Anna Lupembe,Mbunge wa
Jimbo la Nsimbo ametos wito kwa wauguzi wa afya kuzingatia maadili yao ya kazi wanapotoa huduma kwa wananchi pindi
wanapokwenda katika zahanati kutafuta matibabu.
Lupembe amesema kuwa
muuguzi ni karama ambayo wamepewa na Mungu na wanatakiwa kuwa na huruma kwa
wananchi.
Vilevile amewaomba wananchi
kuwa watulivu kwani serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya maji nchini na
kama mbunge anaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha maji safi yanapatikana.