WANANCHI WAUKATIA TAMAA MRADI WA ENEO LA MAONESHO YA KILIMO KATAVI.

Ni jiwe la msingi ambalo lilitumika kama ishara ya uzinduzi wa eneo la Maonesho ya Kilimo katika Kitongoji cha Ikulu Kijiji cha Kabungu Wilaya ya Tanganyika,Kibao cha maandishi kinadaiwa kuchukiliwa na wafungaji wa mifungo ambao hutumia eneo hilo kwa malisho-(Picha na George Mwigulu)

 

Na George Mwigulu, Katavi.

Wazo la kupongezwa limeibuliwa mwaka 2019 na serikali ya Mkoa wa Katavi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa huo,Juma Zuberi Homera (Kwa sasa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya) ni kuanzisha eneo la maonesho ya kilimo (nane nane) ikiwa ni sehemu ya kutambua umuhimu wa historia ya kuanzishwa kwake nchini.

Hapa ni sehemu ya eneo la maonesho ya kilimo ya Mkoa wa Katavi ambapo limeota nyasi na miti mingi kwa sababu ya kutelekezwa kwa muda mrefu

Maonesho ambayo yangebeba dhima kamili kwa wakulima wa Mkoa huo yanaoneka kutelekezwa licha ya faida yake ingekuwa kubwa hasa wanawake na wasichana wangepata fursa ya kuona teknolojia mbalimbali za uzalishaji,usindikaji na masoko pamoja na maarifa na taarifa za kilimo kutoka ndani na nje ya nchi.

Mkoa wa Katavi ni wazi umeshindwa kuzingatia hayo licha ya nia njema ya hapo awali walidhamilia kuanzisha eneo la maonesho ya kilimo licha ya kuwa na maonesho ya kanda jijini Mbeya,Jambo ambalo wananchi wa Mkoa huo kwa muda mrefu wamelipokea kwa furaha.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi zinasema wananchi kuamua kutoa eneo la hekari 240 katika kitongoji hicho ni sauti inayonesha uchungu wa kuhitaji maendeleo na baadhi yao kuamua kutoa ardhi bure kwa serikali bila kudai fidia licha ya kuwa watakosa eneo la uzalishaji kupitia kilimo.

Chanzo hicho kinasema njia ya upatikanaji wa eneo hilo ni baada kupewa elimu na viongozi wa serikali ya Mkoa naye kama kiongozi kwa kushirikiana na viongozi wengine wa ngazi ya kijiji walifanya ushawishi kwa wananchi wote na kukubali.

“ wananchi baadhi yao walitoa bure ardhi na wengine findia ndogo ya Tsh 50.000/=,Tsh 100,000/=,Tsh 200,000/= na wachache ambao walilipwa kwa gharama kubwa kama Tsh 500,000/= kwa sababu walikuwa na nyumba za makazi” Kilibainisha chanzo hicho.

Kutelekezwa kwa mradi huo umekuwa na athari kubwa kwa wananchi baada kuyaachia maeneo hayo na kuhamishiwa kwenye maeneo mengine wakitengemea mradi utakapokamilika fursa ya kukua kiuchumi kwao itapatikana.

“ Watu wamesubilia mradi huo kwa muda mrefu sasa na wamekata tamaa kiasi cha kuuza ardhi zao na kuhama kwenda sehemu zingine ambako wanaweza kupata fursa za kuongeza kipata chao” Ameongeza hayo.

Madhara mengine wamepata wananchi ni baada ya kuchimbwa mtalo mkubwa wa maji kutoka Kitongoji cha Imalausinga hadi Ikulu ambako kutakuwa na eneo la maonesho ya kilimo.Mfereji huo haujajengwa na kusababisha nyumba za makazi kuanguka kwa sababu ya kusambaa maji kwa kasi wakati wa mvua.

“Tumepiga kelele wee ule mtalo analeta maji kwa fosi,ukaleta mmomonyoko mkubwa wa udogo hadi maji kuingia ndani ya nyumba za watu hata sasahivi tutakwenda kuona baadhi maeno ya nyumba zilizoanguka” Amesema bainisha hayo chanzo ambacho jina lake tunalo.

Kiwanda kidogo cha kusanga na kukoboa nafaka kimefungwa kutokana na jengo lake kuwa hatarini kuanguka baada kuzongwa na maji  kwa sababu ya mtalo uliochimbwa kutokujegewa mawe yatakayo zuia maji kusambaa kwa kasi wakati wa mvua.

Huu ni mtalo ambao umechimbwa kwa ajili kupitisha maji kuelekea sehemu ya maonesho ya kilimo,Mtalo huo umelalamikiwa kuwa chanzo cha nyumba za makazi kuaguka kutokana na kutokujengwa hivyo kupitisha maji kwa kasi

Baada ya kufika eneo hilo tumeonana na Anna Sukari,Mkazi wa kitongoji cha Ikulu mama muhanga wa nyumba yake kuanguka kwa sababu ya mfereji kuingiza maji kwa kasi ndani ya nyumba yake anasema “ maji yalikuwa ya kiingia hadi chumbani juu ya kitanda nikiwa nimelala na watoto wangu”.

Mama huyo anaeleza kuwa nyumba yake haikudumu kwa muda mrefu na kuaguka jambo ambalo lilimlazimu kwenda kuomba hifadhi kwa majira zake huku taratibu baadaye alichukua hatua ya kuanza kujenga nyumba nyingine mpya.

Amesema serikali ya Mkoa wa Katavi inapaswa kuujenga mtalo kabla ya mvua za msimu wa kilimo ujao kuanza kunyesha sambamba na kuhuwisha eneo la maonesho ya kilimo (nane nane) kwani wanahisi uchugu kutoa maeneo yao bila kuendelezwa kwa lengo husika.

Mark Sylvester,Mkazi wa Kijiji cha Kabungu anasema serikali ya mkoa wazo lake ni jema na juhudi za awali zinaonyesha kwamba katika sekta ya kilimo wanakwenda kupiga hatua kwani maonesho ya kilimo ni fursa ya kujifunza.

Ni moja ya nyumba zilizoaguka kutokana na mtalo wa maji ambao haujajengwa katika kitongoji cha Ikulu Kijiji cha Kabungu.

Anafafanua kuwa juhudi zilioneka baada ya barabara kuchongwa mitaani,kupelekwa kwa huduma ya umeme na maji safi na salama na baadhi ya taasisi kuanza kuchukua viwanja kwa ajili ya uwekezaji kama vile Shirika la Kuwezesha Wakulima na Wajasiliamali  Katavi tangu mwaka 2021 wamejenga na kuendelea na kazi.

“Maeneo mengine waliweka vibao vya kutambulisha taasisi hizo lakini vibao hivyo hakuna hata kimoja kutokana na wafugaji wa mifungo kufanya eneo hilo la maonesho ya kilimo kama sehemu ya marisho ya mifugo yao” Amesisitiza Mark.

Hata hivyo wananchi wengi wa Mkoa wa Katavi wanauliza maswali “Je mpango wa eneo la maonesho ya kilimo umesahaulika? Na je wazo hilo limebadilika na kuachana nalo?” au kuhama kwa Mkuu wa Mkoa Juma Zuberi Homera na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Muhando kuondoka madarakani ndio wameondoka na mawazo hayo?”.

Magreth  Julius Mkazi wa Manispaa  ya Mpanda, Mjasiliamali kutoka Umoja wa Wasindikaji mbogamboga na matunda.

Magreth Julius,Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi na Mjasiliamali kutoka Umoja wa Wasindikaji Mbogamboga na Matunda (UWAMBOKA) amesema  kuanzishwa kwa eneo la maonesho ya kilimo katika Mkoa wa Katavi kufanikwa kwake itakuwa sehemu ya mapinduzi makubwa ya kitakwimu za kijinsia katika sekta ya kilimo. ili kuchangia katika sera bora na kuinua kiwango cha mipango,ufuatiliaji na uwajibikaji katika sekta hiyo.

Salome Mwasomola,Meneja wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO)Mkoa wa Katavi amesema shirika hilo linatoa huduma ya masoko hasa kuwasaidia wajasiliamali kushiriki maonesho mbalimbali ambapi kwa mwaka 2022/23 wameweza kuhamasisha wajasiliamali  23 ikiwa wanawake ni 17 na wanaume 6 kwenda jijini Mbeya kwenye maonesho ya kikanda ya kilimo.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Katavi,Salome Mwasomola.

Meneja huyo amefafanua faida za maonesho sio tu kukuza mtandao wa kibiashara na kuongeza kipato cha wajasilimali kupitia kuuza bidhaa zao bali inajenga imani kwa watumiaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kutangaza vivutio vya mkoa.

“ wajasiliamali wengi wanashindwa kwenda kwenye maonesho ya kilimo kutokana na kuwa wanapaswa kujighalamia kwa kutumia fedha zao,Suala hilo linapunguza sana ushiriki wa watu hasa wanawake ambao wanamajukumu ya kulea familia zao” Amesema Meneja huyo.

Chanzo cha ndani kinasema ni kweli mipango ya serikali ya Mkoa wa Katavi ni kuanzisha maonesho ya kilimo (nane nane) ambapo zaidi ya hekari 200 zimetengwa na tathimini ya awali ya ujenzi wa jengo maalumu umekamilika ambapo ujenzi wake ni thamani ya Mil 700 zitatumika.

Amesema fedha za ujenzi wa jengo hilo utatokana na michango ya halmashauri ya wilaya za Nsimbo,Mlele,Tanganyika,Mpimbwe,Manispaa ya Mpanda ikiwa kila halmashauri itatoa fedha kulingana na mapato yake ambapo hadi sasa jumla ya fedha  Mil 100.1 zimekusanywa pamoja na fedha zingine kutegemea wadau.

Kutokana na fedha hizo kuwa zimetengwa na utekelezaji wa mradi huo kuchukua muda mrefu ni wazi pasipo na shaka fedha hizo kama sio kwamba ziko hatarini kupotea basi usalama wake wa kuwepo ni mdogo sana kulingana na mwenendo wa hivi karibu baada ya riporti ya CAG kuonesha madudu kwenye halmashauri nyingi hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko anatakiwa kuendeleza mpango wa maonesho  ya kilimo ya mkoa huo kwani kupitia maelekezo ya rais Dkt Samia Suluhu Hassain anahitaji wananchi wengi kushiriki maonesho ya kilimo kwa ajili ya wakulima,wavuvi,wafugaji na wachakataji wa bidhaa mbalimbali waweze kujifunza na kubadilishana uzoefu wa teknolojia.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko

Kwani kuanzisha kwa maonesho ya mkoa utatoa nafasi ya wananchi wengi kushiriki tofauti na sasa ambapo waliokwenda mkoani Mbeya tuliweza kuchukua wananchi takribani kama 225 kutoka halmashauri tano za mkoa wa Katavi.

Mkoa wa Katavi  licha ya kufanya jitihada za kuwa na maonesho yake ya kilimo lakini bado jitihada hazitoshi zinanzofanywa kwa wananchi katika sekta za uzalishaji ambapo mkoa umewahi kufanya maonesho ya siku nne ya bidhaa za kilimo,mifugo,uvuvi, bidhaa za uchakataji na viwanda vidogo vidogo vya wanawake na wasichana.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages