MILIONI 780 KUOKOA WATU KUUWAWA NA MAMBA MTO UGALLA.

 

Hapa ni hifadhi ya taifa ya mto Ugalla uliopo halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Mto huo unasifika kuwa na mamba wengi zaidi ambapo husababisha vifo kwa wananchi wanaokwenda kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya familia.

Na George Mwigulu, Nsimbo.

SERIKALI inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji safi na salama wenye thamani ya fedha ya Mil 780 katika Kijiji cha Katambike kata ya Ugalla Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi.

Ujenzi wa mradi huo umeanza kutekelezwa mwenzi April mwaka huu na unatarajia kukamilika mapema mwenzi Novemba,Hii ni baada ya Katavi Press Club blog kuripoti mara nyingi vifo vya watu wengi hususani wanawake kuliwa na mamba wakati wakienda kuteka maji kwenye hifadhi ya taifa ya mto Ugalla.

Hivyo kukamilika kwa mradi huo utaokoa maisha ya watu kuuwawa na mamba ambapo vifo vyao vimeripotiwa kwa nyakati tofauti.

Halawa Charles Malendeja,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo amesema hayo jana katika kitongoji cha Uvuvini Kijiji cha Katambike Kata ya Ugalla.

Mwenyekiti huyo amesema  kuwa mradi wa maji upo kwenye hatua ya  ujenzi wa tanki la maji lenye ukubwa wa lita laki moja  za ujazo sambamba na uwekaji wa mabomba kwenye maeneo mbalimbali ya kata ya Ugalla unatekelezwa na kampuni ya Planco T Limited.

´´Ninafahamu na ndio maana nikaelekeza na kuomba fedha serikalini ili kuhakikisha tunapata tenki kubwa la maji hapa katika kijiji cha Katambike na kwa sasa ninyi wenyewe mnamuona mkandarasi yupo anaendelea na kazi´´ Amesema Malendeja.

Aidha ameomba RUWASA kupitia gari maalumu ambalo limetolewa na serikali kila Mkoa kuhakikisha wanafika katika  kitongoji cha Uvuvini  na kuwachimbia visima viwili vya maji ambavyo vitasaidia zaidi kuondoa kero maji.

Malendeja amezidi kuiomba serikali kuimarisha miundombinu ya maji ya halmashauri ya Nsimbo kwani wananchi wengi wanakabiliwa na kero ya maji huku sehemu ambayo wanakwenda kuteka ni umbali mrefu zaidi na maji hayo kutokuwa salama.

Baadhi ya wafanyakazi wakichimba mitaro kwa ajili ya kutandazia mabomba ya maji  katika kata ya Ugalla.

anki la maji lenye ujazi wa lita 100,000 likijengwa katika Kijiji cha Katambike Kata ya Ugalla kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama pindi litakapokamilika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Katambike,Shabani Juma Mdaki amesema kuwa wahaga wakubwa wa kuliwa na mamba ni wanawake ambao huenda kuteka maji kwenye mto huo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Wanawake licha ya kuwa hodari na imara zaidi kwenye malezi ya watoto na baba lakini pia ndio wanaohakikisha familia inakula chakula na kunywa maji safi na salama…tizama kitendo cha wanawake kuliwa na mamba kinarudisha nyuma maendeleo ya jamii kwa ujumla” Amesema Mdaki.

Mwenyekiti wa kijiji  hicho amesema "Kwa mwaka 2023 ni zaidi ya watu 14 wameuwawa kwa kuliwa na mamba hii ni takwimu ya mwaka huu ndugu zangu".

Amebainisha kuwa jukumu ambalo wananchi kwa sasa wanapaswa kufanya ni kulinda miundombinu inayowekwa ya maji katika kata ya Ugalla ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya maji safi na salama.

Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa kata ya Ugalla,Mariamu Hassain ameipongeza serikali kwa kazi nzuri ya kuendelea kuhakikisha wananchi wake hawapati matatizo yanayorudisha nyuma maendeleo yao.

Mariamu amesema “… nilishuhudia kwa macho yangu mwanamke mwenzagu akivutwa na Mamba majini na kuliwa na Mamba huyo,Nilipiga kelele licha ya kupata msaada lakini ulikuwa wa kuchelewa sana”.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages