KATAVI IMEONGOZA KUTOA CHANJO YA POLIO II



Na. Zillipa Joseph, Katavi.

Mkoa wa Katavi umetajwa kuongoza katika kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kirusi namba mbili maarufu kama (Polio II) ambapo umeelezwa kufanya vizuri katika kuwafikia walengwa ambao ni watoto wa umri wa miaka sifuri hadi nane huku elimu ya uhamasishaji kwa jamii ikiwa imetolewa kwa kiwango kikubwa.

Hayo yamebainishwa na Afisa Programu Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Bi. Bahati Chipoma alipokuwa mkoani hapa kufanya ufuatiliaji wa zoezi la chanjo ambalo lilifanyika kwa awamu mbili huku awamu ya pili ikiwa novemba 2, 2023.

Bi. Chipoma amesema Wizara ya Afya imelenga kuendelea kutoa elimu jumuishi kwa jamii ili kupata uelewa wa chanjo za magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Polio II.

‘Mkoa wa Katavi umeshika nafasi ya kwanza katika zoezi zima la utoaji wa chanjo ya Polio II kwani imechanja mara mbili ya idadi ya watoto iliyokusudia kuwachanja’ alisema.

Aidha ametoa pongezi kutoka Wizara ya Afya kwa kuwapatia elimu ya kutosha wananchi hali iliyosababisha matokeo mazuri na kuongeza kuwa hakuna taarifa yoyote ya madhara ya chanjo ya Polio II iliyoripotiwa.

Bi. Chipoma ametoa wito kwa wananchi wawe wanawapeleka watoto kupatiwa chanjo pale wanaposikia tangazo na kuongeza kuwa chanjo zingine zinaendelea kutolewa kliniki kwa mujibu wa utaratibu.

Mratibu wa Chanjo mkoa wa Katavi Stephano Kahindi amesema mkoa ulikusudia kuwafikia watoto 227,286 wenye wa miaka sifuri hadi nane na badala yake wamefanikiwa kuwafikia watoto 425,998.

Amesema lengo ni kuwakinga watoto wote waliozaliwa kuanzia mwaka 2016 ambao hawakupata chanjo ya Polio kirusi namba mbili ambayo  ilisitishwa kutolewa na serikali baada ya Tanzania kuutokomeza ugonjwa huo na kuidhinishwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Bwana Kahindi amesema walilazimika kutoa chanjo hiyo kwa awamu mbili kutokana na idadi ya watoto kuwa kubwa kuliko matarajio waliyokuwa nayo.

‘Tulimaliza chanjo na kulazimika kuomba chanjo nyingine kutoka Dodoma’ alisema.

Mchungaji Ibrahim Swalo kutoka kanisa KKKT jimbo la Katavi amesema ni wajibu wa viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Ameongeza kuwa licha ya kuwa ni jukumu la serikali kuhakiskisha watu wake wana afya bora wao wanawajibika kushiriki kuelimisha jamii ili jamii iwe na afya njema.

Ameongeza kuwa umri wa chini ya miaka nane ndipo mtoto anapata nafasi ya kujenga ubongo wake hivyo asipokuwa na afya njema hata ubongo wake hautaimarika ipasavyo na kusisitiza wazazi kuwatoa watoto wapate chanjo ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo polio II.

Bwana Onesmo Buswelu ni Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko aliwataka viongozi wa aina mbalimbali wakiwemo wa kimila na dini kuungana na serikali katika kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa chanjo.

‘Hakuna serikali ambayo inapenda watu wake wateketee, kwa maana hiyo sasa niwatake wananchi watuelewe na kufuata maelekezo yanayotolewa katika maeneo yetu ili kuwalinda watoto wetu’ alisema.

Baadhi ya familia zilizozungumza na mwandishi wa Makala hii wameisifu serikali kwa kuchukua hatua za haraka pindi tatizo linapotokea na kuongeza kuwa suala la kupita nyumba kwa nyumba linasaidia kuwafikia watoto wengi zaidi.

‘Tumesikia kuwa hapo Sumbawanga kuna mtoto alibainika kuugua ugonjwa wa Polio II kwa kweli tunaishukuru serikali kwa kuzinusuru familia zetu´ alisema Abdala Sugaya mkazi wa Kichangani mkoani Katavi.

Zoezi la Chanjo ya polio II awamu ya pili katika mkoa wa katavi ilitolewa kuanzia  Novemba 2-5, mwaka 2023 ambapo zoezi hilo lilifanyika nyumba kwa nyumba, pamoja na kuwafikia watoto waliokuwa mashuleni na kwenye sehemu mbalimbali za kutolea huduma ya afya.

Mikoa mingine iliyoshiriki katika zoezi la utoaji wa chanjo ya polio II kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0-8 ni Rukwa, Kagera, Kigoma, Songwe na Mbeya.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages