WANANCHI TANGANYIKA WALILIA ARDHI YAO WANAYODAI KUPOKWA

 


Na Mwandishi wetu, Katavi.

Wananchi wa zaidi ya kaya 800 wa Kijiji cha  Luhafwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wameiomba serikali kuwasaidia ili wasiondolewe katika  maeneo yao ambayo yako hatarini kupewa mwekezaji.

Wakizungumza jana wawakilishi wa wananchi hao wapatao 30 wa kijiji hicho wametoa kilio chao kwenye kikao walichofanya na waandishi wa habari katika ofisi za Mkoa wa Katavi za ACT Wazalendo zilizopo mtaa wa Nsemlwa-Kichangani Manispaa ya Mpanda.

Masamba Manyama, Mkazi wa kijiji cha Luhafwe wilaya ya Tanganyika amesema kitendo cha serikali ya wilaya hiyo kuwataka kuondoka katika maeneo waliyoishi kwa muda mrefu na kulazimishwa kuhamia mbugani bila kushirikishwa hakikubaliki.

''Naiomba serikali itusaidie kwa sababu tunafahamu Rais wetu anakuja Katavi hili suala watutatulie tumechoka kuteseka kwenye maeneo yetu'' amesema Manyama.

Amebainisha kuwa hapo awali mgogoro huo wa maeneo kati ya wananchi na serikali ya wilaya kutaka maeneo yao kupewa mwekezaji ulikuwa kwenye hatua nzuri ya kutatuliwa wakati wa ziara ya aliyekuwa Katibu wa itikadi, mafunzo na uenezi Paul Makonda lakini baadaye hakuna mafanikio yoyote iliyofikiwa.

Dorikas Sabuni ambaye ni mkazi wa kijiji cha Luhafwe amesema kuwa anashangaa kuona tena viongozi wa wilaya ya Tanganyika kufanya juhudi za kuwatoa katika maeneo yao na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo hapo awali waliondolewa pia.

“Tuliondolewa kwenye maeneo ambayo wanataka kuturudisha tena…tumefika huko na kukuta kuna watu tayari wanaishi je itakuwaje wakati tayari maeneo hayo yanamilikiwa na watu wengine je hii ni maana yake nini au wanataka tugombane sisi kwa sisi ” Amehoji Dorikas.

Amesema kuwa maeneo ambayo wanataka kurudisha kuna kulishuhudiwa ubakaji dhidi yao hapo awali jambo ambalo hadi hivi sasa wana hofu kubwa ya kuhamia kwenye maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Mkoa wa Katavi wa Chama Cha ACT Wazalendo,Joseph Mona amesema wananchi kuondolewa bila ridhaa yao kutoka kijiji cha Luhafwe na kupelekwa Misanga ambalo ni eneo ambalo hapo awali waliweza kuondolewa ni kitendo kibaya.

Mona Amesema kuwa katika eneo la Misanga kuna watu walipoteza maisha kwa kuondolewa kwa nguvu kwa madai kwamba eneo hilo watu hawatakiwi kukaa.

Amemkata Mkuu wa wilaya ya Tanganyika na Mkuu wa Mkoa wa          Katavi kutokukaa kimya bali washughurike mgogoro huo kwa ustawi wananchi wa Luhafwe.

“Kitendo cha wananchi kupewa siku 60 waondoke kwenye maeneo hayo ni unyanyasaji dhidi ya utu wao…..huwezi kusema kwamba sio wakazi wa maeneo ya Luhafwe wakati kwa barua ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika imewahi kukili kwamba hayo ni maeneo ya wananchi” Amesema.

 Raphael Lutoja,Mwenyekiti wa Kijiji cha Luhafwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi baada ya kupigiwa simu alisema kuwa hayuko na hali nzuri ya kulizungumzia mgororo huo kwani amelewa pombe.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages