Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani. |
Na Dan Kimario, Katavi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limejipanga vyema katika kuimarisha usalama wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka krismas na mwaka mpya ili jamii iweze kusheherekea sikukuu hizo katika hali ya amani na utulivu.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani Desemba 24, 2024 .
Kamanda Ngonyani amesema Jeshi hilo limejiwekea mikakati ya kuzuia uhalifu ikiwemo kufanya doria na misako ya masafa marefu na mafupi maeneo mbalimbali na kwa yeyote atakae bainika kuvunja sheria hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake kulingana na uhalifu atakaoutenda.
Aidha, Kamanda Ngonyani amewahimiza wazazi/walezi kuwa karibu na watoto waliochini ya uangalizi ikiwa ni sambamba na kuacha waangalizi majumbani mwao pindi wanapokwenda kwenye ibada na sehemu za starehe ili kuepusha kutokea uhalifu katika maeneo yao.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwakumbusha madereva wa vyombo vya moto kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani na kujiepusha kutumia vileo pindi wanapoendesha vyombo hivyo ili kujiepusha na ajali.
Kwa upande mwengine Kamanda Ngonyani amewataka wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo mengine yenye mikusanyiko kutojaza watu wengi zaidi ya uwezo wa kumbi zao hali itakayopelekea kukosa hewa ya kutosha na kuleta madhara.