![]() |
Na Daniel Kimario -KATAVI
Katika kuadhimisha
kilele cha siku 16 za kupinga ukatili, Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF Net)
Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Dawati la jinsia na watoto wametoa msaada wa
vitendea kazi na vifaa tiba katika zahanati ya Polisi Mkoa wa Katavi.
Akikabidhi vifaa hivyo
Desemba 10, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kamishina Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani amebainisha kuwa Mtandao wa Polisi Wanawake
umetoa vitendea kazi hivyo ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza
chachu katika utoaji huduma kwa wagonjwa wanaohudumiwa na Zahanati hiyo.
Akizungumza baada ya
kupokea msaada huo Mkuu wa kikosi cha Afya Mkoa wa Katavi Mkaguzi Msaidizi wa
Polisi (A/INSP) Dr. Denis Wambura ameushukuru Mtandao wa Polisi wanawake Mkoa
wa Katavi kwa kuguswa kutoa vifaa tiba hivyo ambavyo vitaraisisha utoaji huduma
bora kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma za kiafya katika zahanati hiyo.
Vitendea kazi na vifaa
tiba vilivyokabidhiwa ni pamoja na mzani wa kupima urefu na uzito, kiti cha
maguruduma cha kubebea wagonjwa pamoja na vifaa mbalimbali vya kufanya usafi.