Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Nehemia James akizungumza na washiriki katika mdahalo wa uhuru wa kujieleza.
Na George Mwigulu, Katavi
Wananchi wa Mkoa wa Katavi wameombwa kutumia uhuru wa kujieleza kama nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya nchi.
Maendeleo ambayo yatapatikana kupitia uhuru wa watu kutoa maoni yenye kuleta uwajibikaji sio kwa serikali pekee bali jamii yote kwenye kuibua mahitaji ya jamii na kufuatilia utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Nahemia James, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi amesema hayo Julai 02, 2024 katika ukumbi wa St Mathias Manispaa ya Mpanda wakati akizinduzi semina ya kijamii ya siku moja kuhusu uhuru wa kujieleza unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya ABAROLI na UTPC Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania.
Kaimu Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa jamii ikitumia uhuru wa kujieleza inapaswa kufuata misingi ya kisheria na kuongozwa na uzalendo na haki pasipo kukiuka tamaduni,mila na desturi za nchi ambazo zimekuwa nguvu ya umoja na mshikamano wa Watanzania.
“Waandishi wa habari niwaombe mnapaswa kuzingatia weledi kwenye kazi zenu za kuhabarisha umma kama sehemu yenu ya uhuru wa kujieleza na mfahamu nyie ni kiungo kati ya serikali na jamii” Amesema James.
rais wa UTPC Deogratus Nsokolo akizungumza na washiriki katika mdahalo wa uhuru wa kujieleza. |
Deogratius Nsokolo, rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC amesema kuwa uhuru wa kujieleza unatoa nafasi kwa jamii kuwa na uwezo wa kuhoji na kutoa matatizo yanayoikabili jamii ili wenye mamlaka waweze kuchukua hatua ya kutatua.
rais huyo amefafanua jamii inakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa maji safi, ukatili wa aina mbalimbali kama vile ubakaji na unyanyasaji kwa watoto na wanawake,ubadhilifu wa miradi ya maendeleo ambayo serikali inatumia fedha nyingi kuijenga ambapo yote hayo yatakoma endapo jamii itatumia uhuru wa kujieleza kufichua hali hiyo.
Nsokolo amesema “Nitoe wito kwa wanahabari kushuka katika jamii kuandika habari zinazowagusa na kuepuka mara nyingi kuandika habari za viongozi pekee”.
Keneth Simbaya, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC amefafanua dhima ya uhuru wa kujieleza unaenda sanjali na utekelezaji wa 4Rs za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), Mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding)
4Rs ni msingi imara zaidi kwenye ujenzi wa taifa ambalo lina uhuru wa kujieleza hususani katika kuchochea ustawi wa maendeleo ya watu ambao Rais Dk Samia unausisitiza kila mahala.
Mkurugenzi huyo ameeleza Katiba ya Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayofanyiwa marekebisho mara kwa mara Ibara ya 18 inatoa mambo makuu matatu kuhusu uhuru wa kujieleza.
“Msingi wa Ibara ya 18 unatoa haki ya kujieleza kwenye Kutafuta taarifa,Kupata taarifa na kutoa taarifa” amesema Keneth akisisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa mtu mwingine kuzitoa.
Keneth amefafanua “Mtaanza kuona kwamba hakuna njia ya kuweza kuepuka suala la kutumia uhuru wa kujieleza hivyo kama utakuwa hautafuti utapaswa kutoa hizo taarifa ili wengine waweze kupata hizo taarifa na waitumie kwenye mambo mbalimbali”
Kuhusu mipaka ya uhuru ya kujieleza amesema kuwa kisheri mipaka hiyo inapaswa lazima kuwa imehakikiwa kwenye mipaka ya misingi ya haki na mipaka hiyo itakuwa imepimwa kisheria.
Baadhi ya washiriki wa mdahalo wa uhuru wa kujieleza. |
rais wa UTPC, Deogratus Nsokolo akimkabidhi cheti cha pongeza Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Keneth Simbaya cheti hicho kimetolewa na Katavi Press CLub kama ishara ya kutambua mchango wa UTPC. |
Amesema kuwa kitendo hicho kitaweza kuinua imani ya wananchi kwa Waandishi wa Habari ambayo imeanza kupotea kwa sababu ya kuacha kufuata misingi ya taaluma ya Uandishi wa habari kwa kufuata kuandika habari za wanasiasa huku zikiachwa habari za baadhi ya hosptali kukosa madawa.
Anna Nchagwa, Mwenyekiti wa Taasisi ya shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Katavi ameiomba serikali kujenga miundombuni rafiki ambayo itawawezesha watu wenye ulemavu kutoa maoni yao.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wanauwezo kuwa wa kutoa mchango wa maoni kwa maendeleo ya taifa lao kwa kuwa wanauwezo mkubwa wa kutumia uhuru wa kujieleza kama watapewa nafasi shiriki sawa na watu wengine.
Uzinduzi wa mradi wa semina jamii ya uhuru wa kujieleza Mkoani Katavi umehusisha makundi mbali ya kijamii yakiwemo ya Waandishi wa Habari, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Wanasheria na jamii ili kuchochea ukuaji wa uhuru wa kujieleza kwa maendeleo ya mkoa wao.